Mtalaa wa shahada ya kwanza ya sanaa katika Kiswahili na mawasiliano katika chuo Kikuu cha Egerton unahusu vipengele viwili vinavyohusiana na kukamilishana; yaani lugha na mawasiliano. Jambo hili linalenga kuwatayarisha wanafunzi kupata ujuzi na maarifa yanayowezesha kuhudumu katika nyanja mbalimbali zinazohusu lugha na mawasiliano. Kwa njia hii, mtaala huu unaafikiana na lengo la chuo Kikuu cha Egerton la kuzalisha wasomi wenye ukakamavu na umahiri katika sekta mbalimbali. Mtalaa huu unawalenga wasomi wanaotarajia kuhudumu katika nyanja kama vile habari na utangazaji, ualimu wa lugha, uhariri, uchapishaji, huduma za jamii, tafsiri na fasiri, utafiti n.k.
Mitalaa ya lugha iliyopo kufikia sasa imekuwa ikitilia mkazo lugha bila kuihusisha na mawasiliano. Maendeleo katika nyanja ya teknolojia habari yamezua haja ya wataalam wa lugha wenye upeo mpana, na ambao wana uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazowakumba katika utenda kazi wao. Aidha, ni muhimu lugha ifundishwe kwa kufungamanishwa na utumikizi wake katika nyanja mbalimbali za maisha.
Mwanafunzi wa B.A (Kiswahili na Mawasiliano) katika chuo kikuu cha Egerton ni mwanafunzi wa Kiswahili aliye na kipengele muhimu sana cha mawasiliano ambacho kitampa nafasi bora ya kuwahi kazi katika mashirika mbalimbali yanayoshrikisha mawasiliano katika nyanja mbalimbali kama vile vyombo vya habari, ualimu, mashirika yasiyo ya kiserikali, tafiti mbalimbali, kazi za mawasiliano mema na zile zinazohitaji tafsiri.